UZINDUZI WA DSE SCHOLAR INVESTMENT CHALLENGE 2017

UZINDUZI WA DSE SCHOLAR INVESTMENT CHALLENGE 2017
Leo tarehe 31 Machi 2017 ni siku ya Uzinduzi Rasmi wa Shindano la DSE SCHOLAR INVESTMENT CHALLENGE 2017.
 
DSE SCHOLAR INVESTMENT CHALLENGE ni shindano ambalo limeandaliwa kwa ajili ya Wanafunzi wote wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Shule za Sekondari Nchi Nzima. Shindano hili linaratibiwa na kuendeshwa na Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) kila mwaka kuanzia tarehe 1 Aprili hadi tarehe 30 Juni.
 
Shindano la DSE SCHOLAR INVESTMENT CHALLENGE 2017 limedhaminiwa na CRDB Bank; SWISSPORT Tanzania; na FSDT. Vile vile mfumo wa ushiriki katika hili shindano kwa njia za simu na internet umewezeshwa na Mitikaz Limited na Maxcom Africa.
 
Kwa mara ya Kwanza Shindano la mwaka huu litashirikisha Wanafunzi wa Shule za Sekondari katika Shindano Maalum la Uwekezaji kwa kupitia mfumo wa kiTeknohama unaofikiwa kwa njia ya tovuti ya www.younginvestors.co.tz.
 
Wanafunzi wanaweza kushiriki kwenye hili shindano BURE:

  1. Kupitia tovuti ya www.younginvestors.co.tz
  2. Kupitia Application ya Smartphone ya Leverage Scholar
  3. Kupiga namba ya simu ya *150*36#  

 
DSE imetoa fursa kwa Chuo Cha Uhasibu Arusha ya Kuzindua Rasmi Shindano la Uwekezaji kwa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Shule za Sekondari leo hii.
 
Lengo kuu la Uzinduzi wa Shindano la Uwekezaji la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Shule za Sekondari ni Kuwapa Wanafunzi, Vijana Wetu, Uelewa na Mazoea ya Uwekezaji katika Masoko ya Mitaji na Dhamana.
 
Lengo la DSE la kuelimisha Wanafunzi linapakana na Lengo la Shirika la kimataifa la Child & Youth Finance International. Shirika hili la kimataifa limetenga wiki hii iliyoanza tarehe 27 Machi na kuisha leo hii tarehe 31 Machi kuwa Wiki Rasmi ya Fedha Duniani au Global Money Week kwa mwaka 2017.
 
Wiki ya Fedha Duniani imeratibiwa kwa malengo ya Kuwaelimisha vijana kuhusu:

  1. Haki zao za kijamii na kiuchumi;
  2. Umuhimu wa Kuweka Akiba mara kwa mara, na
  3. Kujiandaa kuingia katika ulimwengu wa sasa wa Kazi na Ajira kwa kushiriki katika fursa mbali mbali za kuelimisha kwa njia ya vitendo.

 
Tunawatakia Wanafunzi watakaoshiriki katika Shindano hili kila la heri katika Uwekezaji wao na pia tunatoa wito kwa Wanafunzi na Wazazi wote Nchini kushiriki katika hili Shindano ili kuongeza elimu kwa Vijana wetu waliopo mashuleni.