DSE CEO SPEECH DURING DSE SCHOLAR INVESTMENT CHALLENGE AWARDS CEREMONY

Hotuba ya Ndg. Moremi Marwa, Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam kwenye Hafla ya Kuwatuza Washindi wa Shindano la DSE Scholar Investment Challenge Tarehe 13/0/2014, - Katika Hoteli ya J.B. Belmonte.
Ndugu Mgeni Rasmi : Bwana Sosthenes Kewe - Technical Director,
Bi. Nasama Masinda -- Afisa Mtendaji Mkuu, Mamlaka ya Masoko ya Dhamana na Mitaji,
Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuuu wa Benki ya NMB
Jopo la Waamuzi (Majaji),
Wageni Waalikwa,
Wandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana,

Kwa niaba ya Soko la Hisa la Dar es Salaam na kwa niaba yangu napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wote kwa kuja katika hafla hizi ya kuwatambua washindi wa DSE Scholar Investment Challenge. Shindano ambalo dhima yake kuu ni kuwafundisha wanafunzi wa elimu ya juu kuhusu uwekaji akiba na uwekezaji katika Masoko ya Hisa na Mitaji kwa njia ambayo ni ya vitendo.

Kama wengi tuanvyojua, kuna dhana na mafikirio kwa wengi wetu katika jamii yetu kwamba uwekezaji katika masoko ya hisa na mitaji ni kwa ajili ya watu wenye upeo fulani wa uelewa au elimu pana juu ya masuala ya fedha, uwekezaji, uchumi na ni pia kuna dhana kwamba uwekezaji huu ni kwa ajili ya watu wenye kipato cha juu. Dhana hii ambayo sio sahihi imejengeka kutokana na kukosa elimu na uelewa juu ya maswala haya na pia umri mfupi wa historia ya uwepo wa Masoko ya Mitaji na Dhamana katika jamii yetu.
Matekoeo ya hali hii na mtazamo huu, ni kwamba baada ya takriban miaka 15 ya uwepo wa soko la hisa na dhamana ni kampuni 19 tu zilizoorodheshwa sokoni (na kati ya hizo 13 tu ndio za ndani) kwa kupata mtaji wa hisa na pia Kampuni kama 10 zilizopata mtaji kwa njia ya hati fungani. Idadi ya wawekezaji pia bado ni ndogo -- kuna wawekezaji takribani laki mbili tu -- idadi ambayo ni chini ya asilimia moja ya Idadi ya watanzania. Na zaidi ya hayo, ukubwa wa mtaji wa Soko kwa kampuni za ndani ni Kama asilimia 16 ya GDP -- ambapo ukubwa jumla wa kampuni hizi ni Shs. 8.7 trillion ukilinganisha na ukubwa wa uchumi yaani GDP ambao unakadiriwa kuwa takribani shs. 54 trillion. Kiwango hiki bado ni kidogo.
Ni kutokana na hali hii ambapo sisi kama Soko la hisa la Dar es Salaam kwa kupitia shindano hili la DSE Scholar Investment Challenge tumeamua kuchukua hatua kujaribu kusaidia kurekebisha Hali hii, na tumeona kuwafundisha vijana wetu walio katika elimu ya vyuo vikuu na kuwahamasisha wao kuelewa dhana hii ya Masoko ya Mitaji na Hisa na kuelewa kwao kutawezesha si tu kwamba siku za mbele uelewa katika jamii utakuwa umeongezeka bali pia hata kwa sasa wao ni chachu kubwa ya uelimishaji wa jamii iwe wazazi wao, ndugu zao, marafiki zao au hata wao wenyewe kuchukua hatua kuwekeza

hicho kipato kidogo walicho nacho. Kwa kufanya hivi jamii yetu kwa ujumla itaondokana na dhana hii potofu ya kutolitumia soko hili kwa maendeleo yetu. Sisi katika soko la hisa tuanaamini kwamba hakuna mahali pazuri ambapo tunaweza kujenga utamaduni wa kubadili mitazamo hii zaidi ya vyuo vya elimu ya juu.
Ni muhimu tungeelewa kwamba utamaduni wa kuweka akiba na uwekezaji, hasa kwa kutumia taasisi za kifedha (iwe mabenki, mifuko ya pensheni, bima na masoko ya hisa na dhamana) pamoja na mifumo mingine ya kifedha bado uko katika kiwango cha chini sana, kiwango hiki bado ni chini ya asilimia 20. Tunayo mengi ya kufanya ili tuweze kukuza kiwango cha matumizi ya huduma za kifedha, na hasa dhamana na mitaji; na moja ya vitu tunavyoweza kufanya ni pamoja na shindano hili ambapo vijana wetu walio katika elimu ya juu kujifunza kwa vitendo jinsi ya kutumia soko la hisa katika masuala ya uwekezaji na hivyo kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza.

Shindano la DSE Scholar Investment Challenge limefanyika kwa kutumia mtandao wa kiteknolojia kwa kupitia simu za mikononi ambapo wanafunzi wameweza kununua na kuuza hisa kwa kutumia virtual capital waliyopewa. Shindano hili, japo huu ndio mwaka wake wa kwanza, litakuwa endelevu likifanyika kila mwaka. Nichukue fursa hii kusema kuwa tumeingia makubaliano na Kampuni ya Smart Youth Limited ya nchini Kenya ili kutumia mtandao wao wa technolojia, ujuzi na uzoefu wao ili kuboresha zaidi shindano hili kwa siku zijazo.
Katika mchakato wa shindano hili, wanafunzi wa elimu ya juu wamepata fursa ya kufanya uchambuzi na utafiti kabla ya kuwekeza na nyingi ya taarifa ambazo wanafunzi wamezitumia ni kwa kupitia mitandao, taarifa zilizo katika vyombo vya habari na pia taarifa zilizo katika mtandao wa soko la hisa; kwa kufanya hivi wameunganisha na elimu ya nadharia waipatayo katika mazingira yao ya vyuo, imewezesha kufikia hatua hii ya leo ambapo baada ya kufanya hatua chache zilizobaki tutakamilisha shindano hili, na washindi watapatikana.

Shindano hili pia limewawezesha wanafunzi kukuza uelewa wao juu ya matumizi ya mahesabu katika biashara, na hususani katika masuala ya fedha, uchumi, uwekaji rasilimali na uwekezaji na pia wanafunzi wameweza kuongeza ujuzi wao wa kufanya uwekezaji katika mazingira ya ushindani, ushirikiano na yenye changamoto. Wanafunzi walipata fursa ya kuwekeza Kama vikundi, kwa wale waliochagua kufanya hivyo, hii pia ilikuwa ni muhimu maana katika mazingira halisi wawekezaji huweka mitaji yao kwa pamoja kwa lengo la kukuza uwekezaji wao na hii nmtandao a ya dhana nzima ya kuwa wanahisa na pia kushiriki katika uwekezaji wa mifuko ya uwekezaji wa pamoja yaani collective investment scheme au pia investment groups.

Wakati wa shindano hili washiriki walipata fursa ya kujifunza na pia kuelewa kwamba mabadiliko ya bei za hisa, na pia tahrisi za soko (yaani stock Index) si tu zinategemea mafanikio ya kifedha na utendaji wa makampuni yaliyoorodheshwa sokoni au utendaji wa sekta ambayo kampuni iliyoorodheshwa imo au hali jumla ya ki-uchumi bali pia mabadiliko hayo yanategemea mtazamo na mafikirio ya wawekezaji (yaani investors' sentiments). Na hii ni dhana ya muhimu sana kwetu Kama jamii na hususan wawekezaji kuelewa.
Kwa maneno mengine, shindano hili limetoa fursa adhimu na ya kipekee kwa wanafunzi walioshiriki kuongeza uelewa, ujuzi na fikra zao juu ya uhalisi wa mazingira ya uwekaji akiba, rasilimali na pia uwekezaji, lakini pia kuelewa mazingira halisi yanayohusu biashara, fedha, uchumi na uwekezaji.

Napenda nitumie fursa hii kuwashukuru kipekee Benki ya NMB na pia wenzetu wa Financial Sector Deepening Trust (FSDT) ambao walitoa mchango muhimu kufanikisha shindano hili, kwa kushiriki kwao kama wadhamini, wamewezesha mafanikio tunayoyashuhudia hapa leo. Pia kipekee niwashukuru Kampuni ya selcom kwa kuandaa mtandao wa kiteknolojia uliowezesha shindano hili kuwezekana, na pia kampuni za simu za Tigo na Airtel ambao katika mitandao hii ya simu wanafunzi waliweza kupata nafasi ya kushiriki shindano hili.
Kwa haya machache – nawashukuruni wote kwa kuja na kushiriki nasi kwenye hafla hii ambapo leo tutakuwa na wasaa wa kuwatangaza washindi watatu ambao watapewa tuzo zao ambazo ni fedha taslimu, vyeti vya ushiriki na kupewa mafunzo kwa vitendo (internship) kwenye soko la hisa la Dar es Salaam au kwa wadau wake.

                                                                                  Ahsanteni sana.